Tarehe mosi mwezi wa kumi China inasherehekea siku ya taifa ambayo pia ni siku ya kuanzishwa kwa China mpya. Katika kipindi hiki kumeshudiwa mabadiliko makubwa yakitokea kwa wanawake ambao hapo awali walionekana wakinyimwa haki zao nyingi pamoja na kutokuwa na suati ya kujitetea kwa lolote lile.
Kwa sasa China ni nchi inayoendelea kila siku, na ambayo ina idadi kubwa ya watu duniani. Kati ya idadi ya jumla ya watu zaidi ya bilioni 1.4 basi nusu yake ni wanawake. Kwahiyo, kuhimiza maendeleo ya wanawake na kupandisha hadhi yao, yamekuwa ni masuala sio yanayopewa umuhimu mkubwa tu kwenye maendeleo ya China, bali pia yanatoa ushawishi mkubwa katika juhudi za kumuendeleza binadamu kwa ujumla.
Katika kipindi chote hicho tangu China mpya iasisiwe mwaka 1949, mwanamke amekuwa akiangaliwa zaidi na kuhakikisha anathaminiwa na kuinuliwa hadi kuwa hadhi sawa na mwanamme. Pamoja na kuendelea kukua kwa uchumi wa China na maendeleo ya jamii kwa ujumla, wanawake wamekuwa wakipewa uhakika zaidi wa kuwa na fursa za kujitambua na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii. Hivyo leo hii kwenye kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia Hadhi ya wanawake ilivyoimarika kwa kiasi kikubwa tangu kuanzishwa kwa China Mpya.