Watu takriban 1,700 wafariki na wengine zaidi ya 12,800 kujeruhiwa katika mvua kubwa iliyonyesha nchini Pakistan
2022-10-03 10:13:57| CRI

Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Majanga (NDMA) nchini Pakistan imesema kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na mvua za monsoon na mafuriko ya msimu huu tangu katikati ya mwezi Juni imeongezeka hadi 1,695 na wengine 12,865 kujeruhiwa nchini humo.

Habari zimesema kuwa watoto 630 na wanawake 340 wamepoteza maisha katika mvua tofauti au ajali zinazohusiana na mafuriko nchini humo.

Aidha, nyumba 2,045,349 ziliharibiwa na mifugo 1,162,122 iliangamia katika maeneo tofauti ya Pakistan. Takriban watu 33,046,329 na wilaya 84 zimeathiriwa na mafuriko. Barabara zenye urefu wa kilomita 13,254.49 na madaraja 440 pia yameharibika katika msimu mzima.

Shughuli za uokoaji na usaidizi za NDMA, mashirika mengine ya serikali, watu waliojitolea na mashirika yasiyo ya kiserikali zinaendelea katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko.