Watu 125 wafariki na wengine zaidi ya 320 kujeruhiwa kwenye mkanyagano uliotokea kwenye uwanja wa soka nchini Indonesia
2022-10-03 10:09:18| CRI

Mkuu wa Polisi nchini Indonesia Jenerali Litsyo Sigit Prabowo amesema, hadi kufikia Jumapili, watu 125 wamethibishwa kufa kwenye mkanyagano uliotokea baada ya mechi ya soka katika mkoa wa East Java nchini Indonesia, na wengine zaidi ya 320 wamejeruhiwa.

Awali, polisi ilisema idadi ya vifo ilikuwa 129 na wengine zaidi ya 180 kujeruhiwa, huku mamalaka ya mkoa ikidai watu waliokufa kwenye ajali hiyo ni 172. Hata hivyo, Jenerali Litsyo amesema baadhi ya majina ya wahanga yaliorodheshwa zaidi ya mara moja.

Mkanyagano huo ulitokea Jumamosi jioni katika uwanja wa Kanjuruhan baada ya klabu ya Arema Malang kupotoza mechi kwa Persebaya Surabaya, kwenye ligi ya soka ya Indonesia. Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimesema mashabiki wa timu iliyoshindwa waliparamia uzio na kuingia kwenye uwanja wa soka na kupelekea mkanyagano na kupambana na polisi, ambapo polisi walirusha mabomu ya machozi yaliyosababisha hofu kwa mashabiki na kuwania kuondoka uwanjani, kitendo ambacho kimesababisha mkanyagano kwenye mlango wa kutokea.

Rais wa nchi hiyo Joko Widodo ameagiza polisi kufanya uchunguzi na tathmini kamili ya utaratibu wa usalama kwenye mechi za soka.