Kenya yaidhinisha mahindi yaliyorekebishwa jeni (GM) kufanywa ya biashara
2022-10-04 10:00:24| CRI

Baraza la mawaziri la Kenya limeidhinisha mahindi yaliyorekebishwa jeni (GM) kufanywa ya biashara na kuruhusu kulimwa na kuagizwa kutoka nje ili kusaidia kuboresha sekta za uzalishaji wa kilimo na viwanda.

Baraza hilo lililoongozwa na rais William Ruto limesema limetoa idhini kama hatua ya kufafanua upya kilimo nchini Kenya kwa kutumia mazao ambayo yana ustahamilivu wa wadudu na magonjwa. Kwa mujibu wa taarifa uamuzi huo ulifikiwa kwa mujibu wa mapendekezo ya kikosi kazi kilichopitia masuala yanayohusu usalama wa chakula na vyakula vilivyorekebishwa jeni, na imani ya muongozo wa Mamlaka ya Taifa ya Usalama wa Viumbe juu ya mikataba yote ya kimataifa ikiwemo Itifaki ya Cartagena ya Usalama wa Viumbe (CPB).

Kenya sasa inajiunga na nchi kama Afrika Kusini, Sudan, Misri na Burkina Faso ambazo zimeruhusu mapema kufanya mazao yaliyorekebishwa jeni yakiwemo mahindi, mtama na kunde pamoja na mazao ya biashara kama vile pamba na maharage ya soya kuwa ya biashara.