Xi awahimiza wafanyakazi wa kijiolojia kubeba jukumu kubwa katika utafutaji wa madini
2022-10-05 09:42:38| CRI

Rasi Xi Jinping wa China ameihimiza timu ya wafanyakazi wa kijiolojia katika mkoa wa Shandong mashariki mwa China kuendeleza desturi nzuri na kubeba jukumu kubwa katika kutafuta rasilimali ya madini.

Rais Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi, aliyasema hayo Jumapili kwenye barua ya kuijibu timu ya wafanyakazi wa kijiolojia ya Bodi ya Jiolojia na Rasilimali za Madini ya mkoa wa Shandong. Kwenye barua yake rais Xi amesema tangu timu ya sita ya wafanyakazi wa kijiolojia wa bodi hiyo ianzishwe, vizazi vya timu hiyo vimefanya juhudi kubwa na kushinda taabu na kuleta matunda katika utafutaji wa rasimali za madini.

Akitaja jukumu muhimu la rasilimali za madini kwenye maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi, rais Xi amesema utafutaji wa rasilimali hii una umuhimu mkubwa katika uchumi wa taifa, maisha ya watu na usalama wa taifa, hivyo amewataka kufanya kazi kwa mtazamo wa maendeleo ya kijani na kuongeza juhudi katika kutafuta rasilimali za madini na kupata mafanikio ya kisayansi ili kutoa mchango katika kulinda nishati ya nchi na usalama wa rasilimali ikiwa ni pamoja na kujenga nchi ya ujamaa wa kisasa katika pande zote.