Juhudi zinazofanywa na walimu mbalimbali wa China na Afrika kwa ujumla
2022-10-07 08:55:14| CRI

Walimu ni vielelezo halisi vya maarifa na hekima, na huwalea na kuwatayarisha wanafunzi kwa ajili ya siku zijazo. Walimu pia ni watu wanaotoa mwanga kwenye dunia ambayo imefifia kwa ujinga. Walimu wetu ndio msingi halisi wa mafanikio yetu. Wanatusaidia katika kupanua ujuzi wetu, kuboresha ujuzi wetu, kupata ujasiri, na kuchagua njia bora zaidi ya mafanikio.

Hivyo kila ifikapo Oktoba 5 dunia inaadhimisha Siku ya Walimu Duniani ili kutambua juhudi zao kote duniani. Siku ya Walimu Duniani pia huadhimishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Elimu Kimataifa.

Tukiangalia historia kidogo ya siku hii ni kwamba Mnamo Oktoba 5, mwaka 1966, Mkutano Maalum wa baina ya serikali za nchi mbalimbali ulikaa na kujadili Hadhi ya Walimu huko Paris. Mkutano huo uliofanyika ili kuchambua masuala yanayowahusu walimu na taaluma yao. Waraka "Mapendekezo kuhusu Hadhi ya Walimu" ulitiwa saini na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na UNESCO. Mapendekezo hayo yanaweka vigezo kuhusu haki na wajibu wa walimu, ambayo pia inasaidia kuboresha elimu kwa kiwango cha juu. UNESCO ikapewa jukumu la kuadhimisha Siku ya Walimu Duniani tangu 1994. Hivyo basi kwenye kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tutaangazia juhudi zinazofanywa na walimu mbalimbali wa hapa China na Afrika kwa ujumla.