Wawekezaji wa Misri waimulika sekta ya viwanda nchini Kenya
2022-10-06 09:48:36| CRI

Balozi wa Misri nchini Kenya Khaled el Abyad amesema mjini Nairobi kuwa Jumuiya ya wafanyabiashara ya Misri ina nia ya kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini Kenya ili kukuza ajenda ya viwanda katika taifa hilo.

Akizungumza kwenye kongamano la biashara kati ya Misri na Kenya, Abyad alisema uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara kati ya pande hizi mbili unahitaji kupanua wigo mbali na mazao ya jadi ya kilimo. Kampuni za Misri zinatafuta fursa kama vile ubia, teknolojia, na mipango ya kuhamisha ujuzi na wenzao wa Kenya, hasa katika eneo la utengenezaji.

Ujumbe wa wafanyabiashara wa Misri wa makampuni 30 uko katika ziara ya siku mbili nchini Kenya kwa ajili ya kushiriki katika mikutano ya pande mbili na wenzao wa Kenya. Ujumbe huo unajumuisha makampuni kutoka sekta ya vifaa vya ujenzi, chuma, saruji, bidhaa za bafuni na sekta za kemikali.

Kwa upande wake, naibu mkurugenzi wa biashara ya kimataifa katika Wizara ya Biashara, Uwekezaji na Viwanda ya Kenya Sylvia Kaburu alisema serikali ya Kenya inaweza kuendeleza sekta ya viwanda yenye ushindani kupitia ushirikiano na wanaviwanda wa kigeni.