Waziri wa afya wa Tanzania akagua kazi za kujiandaa kupambana na Ebola katika maeneo ya mpakani na Uganda
2022-10-06 09:52:20| CRI

Waziri wa Afya wa Tanzania Bi. Ummy Mwalimu ametembelea maeneo ya nchi hiyo yaliyopo mpakani na Uganda ili kukagua hali ya maandalizi na mipango ya dharura ya kudhibiti mlipuko wa Ebola uliotokea katika nchi jirani ya Uganda.

Katika ziara yake wilayani Missenyi mkoani Kagera, waziri huyo amewataka wananchi waishio mpakani kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo hatari, na kuongeza kuwa hadi sasa Tanzania hakuna mgonjwa aliyeripotiwa kuwa na Ebola.

Amesema kuwa katika nchi hizo mbili jirani wamekataa kufunga mipaka yao lakini watu wanapaswa kuzingatia kuchukua hatua muhimu za kuzuia ugonjwa huo. Mikoa mitano iliyo karibu na Uganda ina sehemu za kuingilia mpakani ambazo zinaweza kutoa mianya kwa watu wenye ugonjwa huo kuingia nchini bila kutambuliwa.

Aliagiza mikoa kuandaa haraka mipango ya dharura, ikiwemo dharura ya afya ya umma na timu za kukabiliana kwa haraka ili kuwa tayari kwa tukio lolote.