China yatoa wito wa kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza uwezo wa kusimamia maliasili
2022-10-07 09:44:33| CRI

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Dai Bing ametoa wito wa kusaidia serikali za nchi za Afrika kuimarisha uwezo wao wa kusimamia maliasili, ili kukabiliana na biashara haramu ya maliasili na kunufaika nayo kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza kwenye mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wenye mada "Amani na Usalama Barani Afrika: Kuimarisha Mapambano Dhidi ya Ufadhili wa Makundi yenye Silaha na Magaidi Kupitia Usafirishaji Haramu wa Maliasili", Bw. Dai amesema katika baadhi ya maeneo yenye migogoro barani Afrika, vitendo vya uendelezaji na usafirishaji haramu wa maliasili, wakiwemo wanyamapori vimekithiri na kunufaisha makundi yenye silaha na vikosi vya kigaidi, na hivyo kuwa kichochezi cha migogoro. Amesisitiza kuwa uwezo ulioimarishwa wa utawala unaweza kuziba kwa ufanisi mianya ya usafirishaji haramu wa rasilimali kwa faida haramu.

Ameeleza kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuunga mkono kikamilifu jukumu kuu la serikali za nchi za Afrika katika usimamizi wa rasilimali, na kusaidia nchi zilizoathiriwa na migogoro kuboresha uwezo wao katika mipango ya viwanda, usimamizi wa fedha na utekelezaji wa usalama ili kuwezesha utajiri wa rasilimali zao kuleta maendeleo.