Kura ya maoni kuhusu suala la Xinjiang yashindwa kwenye Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa
2022-10-07 15:37:39| CRI

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China ametaka nchi za magharibi hasa Marekani ziache kuichafua na kuikandamiza China katika suala la Xinjiang, na kuchukua hatua halisi kwa ajili ya maendeleo ya haki za binadamu duniani.

Msemaji huyo ameyasema hayo alipohojiwa kuhusu muswada wa suala la Xinjiang uliotolewa na Marekani kushindwa kwenye kura za maoni za Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa. Amesema kwa muda mrefu sasa, nchi za magharibi ikiwemo Marekani mara kwa mara zimetoa kauli zisizo za kweli kuhusu masuala ya Xinjiang, na kujaribu kuichafua China kwa kisingizio cha haki za binadamu, ili kuzuia maendeleo ya China.

Msemaji huyo amesisitiza kuwa suala la Xinjiang si suala la haki za binadamu, bali ni suala la kupambana na ugaidi, msimamo mkali na ufarakanishaji. Amesema katika miaka ya hivi karibuni, karibu nchi 100 duniani zikiwemo za Kiislamu zimetoa sauti, zikiunga mkono msimamo wa China katika suala la Xinjiang, na kupinga vitendo vya kuingilia mambo ya ndani ya China kupitia suala hilo.