Idadi ya vifo kutokana na ufyatuaji risasi katika kituo cha kulelea watoto nchini Thailand yaongezeka hadi 38
2022-10-07 09:41:55| CRI

Idadi ya vifo kutokana na shambulizi la ufyatuaji risasi katika kituo cha kulelea watoto cha mkoa wa Nong Bua Lamphu, kaskazini mashariki ya Thailand imeongezeka hadi 38, wengi wao wakiwa watoto.

Mkuu wa Polisi wa Kitaifa Bw. Damrongsak Kittipraphat amesema kuwa mshambuliaji huyo alikuwa afisa wa zamani wa polisi ambaye alikamatwa mapema mwaka huu kwa tuhuma za dawa za kulevya na kufukuzwa kazi mwezi Juni, ambapo alitakiwa kujibu mashtaka ya dawa za kulevya mahakamani siku ya Ijumaa.

Bw. Damrongsak amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari saa chache baada ya tukio hilo. Ameongeza kuwa wakati mshambuliaji huyo anavamia kituo cha kulelea watoto, wanashuku kwamba alikuwa ametumia dawa za kulevya na kuwa na msongo wa mawazo kutokana na kesi inayokuja.

Waziri Mkuu wa Thailand Prayut Chan-o-cha aliandika kwenye mtandao wa kijamii akitoa rambirambi zake za dhati kwa familia za watu waliofariki na majeruhi, pia alimuamuru mkuu wa polisi wa taifa kufanya uchunguzi haraka.