Kenya yachukua hatua ya kuhimiza utatuzi wa mgogoro wa kibiashara
2022-10-07 09:43:05| CRI

Muungano wa Sekta Binafsi wa Kenya (KEPSA) na Kituo cha Nairobi kinachoshughulikia usuluhishi wa kimataifa (NCIA) wamesaini kumbukumbu ya maelewano kwa ajili ya kuhimiza utatuzi wa mgogoro wa kibiashara.

KEPSA ilitoa taarifa ikisema mashirika hayo mawili yatafanya ufumbuzi mbadala uwe njia kuu ya kutatua mgogoro wa kibiashara, na kuzihamasisha sekta binafsi ziepuke kuwasilisha madai ya gharama kubwa, hali ambayo inaashiria mazingira mabaya ya uwekezaji.

Ofisa mkuu mtendaji wa KEPSA Carole Kariuki alisema makubaliano hayo yatasaidia kutatua mgogoro wa kibiashara kwa amani, na kuchochea uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa kituo cha NCIA Lawrence Ngugi alisema Afrika inapendelea zaidi kuchukua ufumbuzi mbadala katika kutatua mgogoro wa kibiashara badala ya kuwasilisha madai mahakamani kutokana na ongezeko la biashara ya kimataifa, uwekezaji na uvumbuzi wa kibiashara barani humo.