Mawaziri wa kilimo wa nchi za Pembe ya Afrika wataka mabadiliko ya sera ili kuondokana na mgogoro wa njaa
2022-10-10 08:59:39| CRI

Mawaziri wa kilimo wa nchi za Pembe ya Afrika wamesema, mageuzi makubwa katika sera za kilimo zilizopo sasa, uwekezaji bora, teknolojia na utafiti ni muhimu katika kumaliza mgogoro wa njaa katika kanda hiyo.

Wakizungumza katika warsha iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) na kufanyika jijini Nairobi, Kenya, mawaziri hao wamesisitiza kuwa, kuondokana na ukosefu wa usalama wa chakula katika kanda hiyo kunategemea kasi ya mageuzi ya mifumo ya kilimo kuwa inayozingatia hali ya hewa na kilimo cha kibiashara.

Katibu Mkuu wa IGAD, Workneh Gebeyehu amesema, mishtuko inayotokana na mabadiliko ya tabianchi, mapigano, uvamizi wa nzige wa jangwani na vita ya Ukraine vimeongeza njaa na utapiamlo katika kanda hiyo, na kuwa kikwazo cha ukuaji na utulivu endelevu. Ameongeza kuwa, zaidi ya watu milioni 51 katika nchi saba kati ya nane wanachama wa Shirika hilo wanakadiriwa kuwa na hali mbaya ya chakula, na wengine 388,000 wako hatarini kukabiliwa na njaa.