AfCFTA yazindua mwongozo wa mapendekezo ya biashara kwa nchi saba
2022-10-10 08:58:50| CRI

Sekretarieti ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA) iliyoko mjini Accra, Ghana, imezindua mwongozo wa mapendekezo ya biashara kwa nchi saba wanachama zilizoonyesha utayari wa kufanya biashara chini ya Eneo hilo, ambazo ni Tanzania, Mauritania, Kenya, Misri, Cameroon, Rwanda na Ghana.

Katibu mkuu wa Eneo hilo Wamkele Mene amesema, karibu asilimia 96 ya bidhaa kutoka nchi hizo saba zinaweza kuuzwa kwa uhuru chini ya kanuni za AfCFTA. Bidhaa ambazo zimepitishwa kuuzwa chini ya Eneo hilo ni pamoja na bidhaa za mbogamboga, dawa, vyombo vya jikoni, sukari, chuma na bidhaa za mbao.

Waziri wa Biashara na Viwanda wa Ghana Alan Kyerematen amesema, kuzinduliwa kwa mwongozo huo wa biashara kati ya nchi hizo saba kunaashiria kuwa AfCFTA ni halisi, na pia ni ishara kuwa serikali za nchi za Afrika zilizohusika katika majadiliano kwa sasa zinatoa njia kwa sekta binafsi kufanya eneo hilo kuwa uhalisia.