Mashirika ya Umoja wa Mataifa yatoa wito wa uwekezaji katika afya ya akili barani Afrika
2022-10-11 08:44:28| CRI

Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) yametoa wito kwa uwekezaji zaidi katika huduma za afya ya akili barani Afrika, ambako janga la COVID-19 limeweka wazi pengo lililopo katika huduma ya afya ya akili.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa jijini Nairobi, Kenya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Afya ya Akili, Mashirika hayo mawili yameahidi kushiriki kwa pamoja katika hatua za kutoa kipaumbele katika afya ya akili.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Bi. Matshidiso Moeti amesema, afya ya akili ni muhimu sana kwa ajili ya afya na ustawi. Amesema changamoto kubwa kwa utoaji wa huduma ya afya ya akili barani Afrika ni uwekezaji mdogo wa serikali katika sekta hiyo, na kuongeza kuwa huu ni wakati mwafaka wa kufanya mabadiliko makubwa.