Malawi yapiga marufuku mauzo ya chakula katika shule za msingi na sekondari ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu
2022-10-11 08:41:06| CRI

Malawi imepiga marufuku mauzo ya chakula katika shule za msingi na sekondari katika mwaka ujao wa masomo ulioanza jana jumatatu, wakati mlipuko wa kipindupindu ukisababisha vifo vya watu 117 mpaka kufikia jumapili iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Wizara ya Elimu nchini humo Chikondano Mussa imewataka wazazi kuwafungashia watoto wao chakula kinachopikwa nyumbani, na kuzuia mauzo ya chakula katika shule mpaka itakapotangazwa baadaye.

Taarifa hiyo pia imeshauri kuwa vyuo vikuu na vyuo vingine vinapaswa kuhakikisha kuwa wauzaji na wasambazaji wa vyakula wanafuatilia na kutekeleza mchakato wa utendaji uliotolewa na Wizara hiyo kwa taasisi zote za elimu.

Ugonjwa wa Kipindupindu umeendelea kuenea nchini Malawi tangu kesi ya kwanza iliporekodiwa katika mkoa wa Machinga, kusini mashariki mwa nchi hiyo mwezi Machi mwaka huu.