Umoja wa Mataifa watoa wito wa kusimamisha mapigano nchini Sudan Kusini
2022-10-12 08:24:55| CRI

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kusimamishwa mara moja kwa mapigano wakati mapigano yakiendelea kati ya makundi yenye silaha katika Kaunti ya Fashoda mkoa wa Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na masuala ya Sudan Kusini ambaye pia ni kiongozi wa Tume ya Umoja wa Mataifa nchini humo, Nicholas Haysom amewataka viongozi wote wa kisiasa, kijamii, dini na makabila, kumaliza vurugu na kurejesha usalama katika jamii zilizoathirika.

Amesema mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa, wanawake kutekwa nyara, na zaidi ya watu 8,000 kukimbia makazi yao kutoka Mji wa Kodok na maeneo ya jirani na kuongeza kuwa, juhudi za kupeleka misaada ya kibinadamu katika maeneo hayo zinakwama kutokana na ukosefu wa usalama.