Watu watatu wafariki na wengine 74 waugua nchini Tanzania baada ya kula nyama ya kobe
2022-10-13 08:24:42| CRI

Watu watatu wamefariki na wengine 74 kuugua baada ya kula nyama ya kobe inayoshukiwa kuwa na sumu katika mkoa wa Lindi, kusini mwa Tanzania.

Daktari Mkuu wa mkoa huo Khery Kagya amesema, watu hao wanashukiwa kula nyama ya kobe yenye sumu katika kijiji cha Rushungu, mkoa wa Kilwa, wiki moja iliyopita. Amesema wavuvi waliwauzia wanakijiji nyama hiyo ya kobe bila ya wao kujua, na wanakijiji hao waliugua saa chache baada ya kula nyama hiyo, ambapo walianza kutapika mfululizo huku wengine wakipata maumivu makali ya tumbo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi Pili Mande amesema, polisi wameanza uchunguzi juu ya tukio hilo.

Serikali ya Tanzania imepiga marufuku ulaji wa nyama ya kobe kwa lengo la uhifadhi wa wanyama hao, lakini baadhi ya wavuvi wanauza nyama hiyo kwa njia zisizo halali.