Mara nyingi kumekuwa na nadharia ama mtazamo kuwa, baadhi ya kazi ni maalum kwa wanaume tu, na wanawake hawana uwezo wa kufanya kazi husika. Ni sawa tu na masomo ya sayansi ambayo inaaminika kuwa wanaume ndio wanayamudu zaidi ya wanawake. Lakini mwenendo wa zama hizi umeonyesha kwamba, wanawake wanaweza kufanya kazi sawa n ahata kuwazidi wanaume katika zile kazi ama masomo yanayochukuliwa kuwa ni ya wanaume.
Hii inadhihirika kutokana na wanawake kuonekana katika sekta nyingi ambazo awali zilikuwa zinachukuliwa kuwa ni za wanaume. Kuna wanawake marubani, wahandisi, madereva wa mabasi ya umbali mrefu, madereva wa treni, na pia wanasayansi wanaofanya mambo makubwa katika sekta husika. Wanawake wameonyesha uwezo wao wa kumudu kazi ngumu na kuzifanya kwa ufanisi mkubwa, na hivyo kuwa chachu kwa wanawake wengine kutokuwa na hofu na kujiamini kuwa wanaweza. Katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii, tutaangazia jinsi wanawake walivyojikomboa na kuingia katika kazi ambazo awali zilidhaniwa kuwa zinaweza kufanywa na wanaume pekee.