Mkutano Mkuu wa 20 wa wajumbe wote wa CPC kufunguliwa kesho asubuhi
2022-10-15 19:08:15| CRI

Msemaji wa Mkutano Mkuu wa 20 wa wajumbe wote wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Sun Yeli leo ametangaza kuwa Mkutano huo utafunguliwa kesho asubuhi saa 4 kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, na utafanyika hadi tarehe 22, na maandalizi yote yamekamilika.

Bw. Sun amesema baada ya kuchunguzwa na Kamati ya Uchunguzi wa Mkutano huo, wajumbe 2,296 watawawakilisha wanachama zaidi ya milioni 96 wa CPC kuhudhuria mkutano huo.

CPC yenye historia ya miaka 101, ni chama kikubwa zaidi cha kisiasa duniani. Mkutano wake wa wajumbe wote unafanyika kila baada ya miaka mitano. Kwenye mkutano huo, wajumbe watajadili ripoti za awamu iliyopita za Kamati Kuu ya Chama na Kamati ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Chama, kurekebisha katiba ya Chama, kujadili na kuamua masuala muhimu ya Chama, na kuchagua wajumbe wa awamu mpya ya Kamati Kuu ya Chama na Kamati ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Chama.