Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambacho ni chama tawala cha China umefunguliwa leo saa nne asubuhi mjini Beijing, na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 2,300 wa wanachama wa CPC. Mkutano huo utafanyika kuanzia leo hadi tarehe 22, Oktoba.
Mkutano huo utasikiliza na kuthibitisha ripoti ya Kamati Kuu ya 19 ya CPC, na ripoti ya Kamati ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Kamati Kuu hiyo, kuthibitisha na kupitisha Marekebisho ya Katiba ya Chama, na kuchagua na kuunda awamu mpya ya Kamati Kuu ya Chama na Kamati ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Kamati Kuu hiyo.
Tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, Chama cha Kikomunisti cha China chenye historia ya miaka 101 kimeendelea kutawala nchi hiyo kwa miaka 73, kikiwa na wanachama zaidi ya milioni 96. Mkutano Mkuu wa Wajumbe Wote na Kamati Kuu ya Chama inayochaguliwa kwenye mkutano huo, ni mamlaka za juu zaidi za uongozi za CPC, na Mkutano Mkuu wa wajumbe wote wa CPC unafanyika kila baada ya miaka mitano.