Mkutano mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China wafunguliwa Beijing
2022-10-17 09:07:06| CRI

 Mkutano mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) umefunguliwa rasmi asubuhi ya Jumapili hapa Beijing.

Xi Jinping alitoa hotuba kwenye mkutano huo kwa niaba ya kamati kuu ya 19 ya CPC yenye kichwa “Kunyanyua Juu Bendera ya Ujamaa wenye Umaalum wa China, Kushikamana kwenye Jitihada za Kujenga Nchi ya Kisasa ya Kijamaa Kwa Pande Zote”.

Xi amebainisha kuwa, mkutano mkuu wa 20 wa CPC ni mkutano muhimu unaofanyika wakati Chama kizima na watu wa makabila yote ya China wanaanza safari mpya ya kuijenga China kuwa nchi ya kisasa ya kijamaa na kusonga mbele kuelekea kwenye Lengo la Pili la Miaka 100.

Wakati wa majumuisho ya kazi zilizofanywa katika muongo uliopita, Xi amesema katika miaka kumi iliyopita, watu wa China wameshuhudia mambo makubwa matatu yenye umuhimu mkubwa katika zama hii na historia kwa Chama na wananchi: kwanza ni kutimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwa CPC; pili ni Ujamaa wenye umaalum wa China kuingia kwenye zama mpya; tatu ni kukamilisha jukumu la kihistoria la kutokomeza umaskini uliokithiri na kukamilisha ujenzi wa Jamii yenye Maisha Bora, na hivyo kufikia Lengo la Kwanza la Miaka 100. Amesema huu ni ushindi wa kihistoria uliopatikana kwa juhudi za pamoja za Chama na wananchi, ni ushindi wa kihistoria unaong’ara kwenye historia ya maendeleo ya taifa la China, na pia ni ushindi wa kihistoria unaotoa athari za kina kwa dunia nzima.

Akizungumzia jukumu la CPC katika zama mpya na kwenye safari mpya, Xi ameainisha kuwa kuanzia sasa, jukumu kuu la Chama ni kuwaunganisha na kuwaongoza watu wa makabila yote katika kuijenga China kuwa nchi ya kisasa ya kijamaa, kufikia Lengo la Pili la Miaka 100, na kusukuma mbele ustawishwaji wa taifa la China kwa njia ya kisasa ya kichina.