Xi Jinping atoa hotuba muhimu kwenye kikao cha ufungaji cha Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC
2022-10-22 22:30:42| cri

Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) umefungwa tarehe 22 hapa Beijing. Kwenye ufungaji wa mkutano huo, wajumbe 2,338 walipiga kura kuchagua Kamati Kuu mpya ya CPC na Kamati Kuu mpya ya Ukaguzi wa Nidhamu, na kupitisha azimio kuhusu ripoti ya kazi ya Kamati Kuu ya 19 ya CPC, azimio la ripoti ya kazi ya Kamati Kuu ya 19 ya Ukaguzi wa Nidhamu, na azimio la marekebisho ya Katiba ya CPC.

Mkutano huo umekubali kuyaongeza kwenye katiba ya Chama maendeleo mapya ya kinadharia katika Fikra ya Xi Jinping kuhusu Ujamaa wenye Umaalum wa China katika Zama Mpya tangu Mkutano Mkuu wa 19 wa CPC, na kurekebisha na kuboresha maelezo kuhusu malengo ya kufikiwa kwenye Katiba kwa mujibu wa majukumu makuu ya CPC yaliyotajwa kwenye Mkutano Mkuu wa 20. Pia umebainisha malengo ya kimkakati ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ya kutimiza mambo ya kisasa ya ujamaa ifikapo mwaka 2035 na kuijenga China kuwa nchi ya kisasa ya ujamaa yenye nguvu ifikapo katikati ya karne hii, yaani kutimiza “Lengo la Pili la Juhudi za Miaka 100”.

Kwenye kikao cha ufungaji alichoendesha siku hiyo, Xi Jinping pia alitoa hotuba akisisitiza kuwa baada ya juhudi za karne nzima, CPC kwa mara nyingine kinaanza safari mpya, ambayo itakuwa na mitihani mipya. Amesema chama hicho kinajiamini kikamilifu na kinaweza kuunda miujiza mipya na mikubwa zaidi katika safari mpya ya zama mpya ambayo itaishangaza dunia. Ametoa wito kwa Chama kizima kuendelea na juhudi za kuwaunganisha na kuwaongoza Wachina wote katika kujitahidi kujenga China kuwa nchi ya kisasa ya ujamaa na kustawisha taifa la China.