China itahimiza maendeleo yenye ubora wa juu ili kutoa fursa zaidi kwa dunia
2022-10-23 15:04:13| CRI



China itafuata kithabiti sera ya kuimarisha mageuzi na kufungua mlango, na kuhimiza maendeleo yenye ubora wa juu ili kutoa fursa zaidi kwa dunia.

Hayo yamesemwa na Bw. Xi Jinping leo hapa Beijing alipokutana na waandishi wa habari baada ya kuchaguliwa tena kuwa katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China CPC, akiongozana na wajumbe wengine wa kamati ya kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya 20 ya CPC. Bw. Xi amesema hivi sasa, China inaanza safari mpya ya kujenga nchi ya kisasa ya kijamaa kwa pande zote, kuelekea “Lengo la pili la Juhudi za Miaka 100”, na kutimiza ustawishaji wa taifa la China kwa njia ya China ya kujiendeleza kisasa. Uchumi wa China ni thabiti, una nguvu za kutosha ambazo hazijatumiwa ipasavyo, na una uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto, na kwamba hali ya kimsingi ya kukua kwa muda mrefu haibadiliki.

Xi Jinping amesema njia ya China kujiendeleza kisasa ni matokeo ya majaribio ya muda mrefu ya CPC na watu wa China, na ni kazi kubwa na ngumu. Katika safari mpya, Chama daima kitafanya kila kitu kwa ajili ya watu na pia kuwategemea watu, na kubadilisha matarajio mema ya watu na maisha bora kuwa halisi.

Xi Jinping amesisitiza kwamba CPC daima itahimiza mapinduzi binafsi, na kuhimiza usimamizi mkali wa Chama kwa pande zote, ili Chama hicho chenye historia ya zaidi ya miaka 100 kiendelee kuwa na uhai, na daima kiwe nguvu ya kuaminika ya watu wa China.

Xi Jinping amesema, licha ya changamoto kubwa zinazoikabili dunia hivi sasa, CPC imekuwa ikishikilia kwamba hatma ya binadamu inapaswa kushikiliwa na kuamuliwa na watu wa nchi zote duniani. Iwapo dunia inafanya kazi pamoja, nchi zote zitaweza kuishi kwa mapatano, kufanya ushirikiano wa kunufaishana na kujenga siku nzuri za dunia. Amesema maendeleo ya China hayatenganishwi na dunia, na maendeleo ya dunia pia yanaihitaji China. China itashirikiana na nchi nyingine zote kutetea maadili ya pamoja ya binadamu ya amani, maendeleo, usawa, haki, demokrasia na uhuru ili kulinda amani ya kimataifa na kuhimiza maendeleo ya dunia, na kuendelea kukuza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.