Vikosi vya Somalia vyawaua wapiganaji wa al-Shabaab zaidi ya 100 katika operesheni
2022-10-25 09:04:35| CRI

Vikosi vya usalama nchini Somalia vinavyooungwa mkono na washirika wa kimataifa, vimewaua zaidi ya wapiganaji wa al-Shabaab 100 na wanamgambo wao katika opresheni za siku mbili zilizofanyika katikati ya nchi.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Utalii, Abdirahman Adala amesema operesheni hizo ambazo ziliwalenga viongozi wa al-Shabaab na wanamgambo wao (Khawarji) pia zimeharibu vifaa vya vilipuzi vinavyobebwa na magari. Amesema operesheni hizo zilizofanikiwa zilifanywa kwa ushirikiano na Shirika la Ujasusi la Kitaifa na Usalama (NISA) pamoja na washirika wa kimataifa katika maeneo ya Masajid Ali-gud na Burolow, katika mkoa wa Shabele ya Kati.

Vikosi vya usalama vimeapa kuimarisha opereseheni za anga na ardhini ili kuwatoa wapiganaji wa al-Shabaab ambao wanashambulia wenyeji na kukusanya kodi kinyume cha sheria kutoka kwa wakaazi.