Utaratibu wa pande tatu wasisitiza kulinda usalama wa waandamanaji wa Sudan kwenye maandamano yatakayofanyika karibuni
2022-10-25 08:54:23| CRI

Utaratibu wa pande tatu unaoshughulikia kurahisisha mazungumzo ya ndani ya Sudan umehimiza vikosi vya usalama vya Sudan viwalinde waandamanaji kwenye maandamano yanayotazamiwa kufanyika leo hii.

Utaratibu huo wa pande tatu unaoundwa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) ulitoa taarifa ukivitaka vikosi vya usalama vijizuie na kulinda uhuru wa waandamanaji wa kujieleza, kuungana na kukusanyika kwa amani.

Utaratibu huo ulisisitiza kuwa ufumbuzi wa kisiasa unahitajika sana ili kuondoa mvutano unaoikumba nchi hiyo hivi sasa, na kuunda serikali halali ya kiraia, kurejesha usalama na utaratibu wa katiba.