Wataalamu wataka kuchukuliwa hatua za kuzuia msukosuko wa kiuchumi katika Afrika
2022-10-26 09:50:58| CRI

Wataalamu wa mambo ya fedha wametoa wito wa kutekeleza kwa ufanisi hatua za kuzuia msukosuko wa kiuchumi katika Afrika.

Akiongea kwenye mjadala kuhusu Mtazamo wa Uchumi wa Kikanda wa IMF, Catherine Pattillo, naibu mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) jana alisema mjini Nairobi, Kenya, kuwa kushuka kwa uchumi pamoja na kupanda kwa bei ya chakula na nishati huenda ikaleta athari kwa wakaazi wa maeneo yaliyo hatarini zaidi. Ameeleza kuwa watunga sera wa Afrika wanapaswa kuweka kipaumbele katika hatua zitakazopiga jeki usalama wa jamii kama moja ya maeneo ambayo yatafufua uchumi endelevu. Pia amesema utekelezaji wa uimarishaji wa mambo ya fedha utasaidia kupunguza nakisi ya bajeti pamoja na gharama za mikopo ya nje.

Naye gavana wa Benki Kuu ya Kenya Patrick Njoroge amesema uratibu mzuri wa fedha za ndani na kigeni utasaidia Afrika kuondokana na sera mbaya ya sarafu kimataifa ambao unaipa shinikizo kubwa thamani ya sarafu za nchi za Afrika.