Mkuu wa UNHCR aonya juu ya migogoro isiyoonekana katika Pembe ya Afrika
2022-10-26 09:52:33| CRI

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Bw. Filippo Grandi ametoa wito kwa viongozi duniani kujitahidi kuzisaidia nchi za Pembe ya Afrika kuondokana na vurugu na misukosuko ya hali ya hewa inayojirejea mara kwa mara.

Bw. Grandi amesema hayo baada ya kumaliza ziara yake ya siku tano nchini Somalia na Kenya, ambapo ameonya katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, kwamba maafa na athari nyingi katika eneo hilo hazionekani kwani dunia imeelekeza macho yake kwenye maeneo mengine.

Takwimu mpya za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa idadi ya watu waliokimbia makazi yao mwaka huu nchini Somalia, hasa kutokana na ukame inakaribia milioni 1, na wengine wapatao laki 5 wamehama makazi yao kutokana na migogoro na ukosefu wa usalama.

Ameongeza kuwa athari za ukame nchini Kenya haziko kwenye vichwa vya habari, lakini zinastahili kuzingatiwa sana na jumuiya ya kimataifa. Amesema lazima wapate rasilimali za kuhudumia zaidi watu waliowasili Afrika kutoka Somalia na vilevile Wakenya walioathiriwa.