Ushirikishwaji wa Wanawake kwenye Siasa
2022-10-28 08:00:29| CRI

Takwimu zinaonesha kuwa uwanja wa siasa katika nchi nyingi umetawaliwa na idadi kubwa ya wanaume ikilinganisha na wanawake. Hali hii imetokana na mfumo dume ambao umegawa majukumu katika jamii kulingana na jinsia. Katika mgawanyo huu wanawake wameegemea zaidi kwenye masuala yanayohusu malezi na utunzaji wa familia na kazi za nyumbani. Wanaume nao wameelekezwa zaidi kwenye uwanja wa siasa na hata kuhesabiwa kama ndio viongozi wakuu.

Kutokana na mgawanyo huu hapo zamani ilikuwa vigumu kwa wanawake kuingia kwenye uwanja wa siasa na hasa katika ngazi mbalimbali za uongozi. Mgawanyo huu umedumu kwa miaka mingi na umepelekea kuzaa hali ya kutokuwepo na usawa kati ya wanawake na wanaume, utengwaji au kutengwa, unyanyasaji wa kijinsia.

Mbali na mfumo dume, kuna baadhi ya mambo mengine mengi yaliyochangia katika kutokuwepo na usawa katika uwiano wa wanawake na wanaume katika uwanja wa siasa hasa katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi. Baadhi ya mambo hayo ni kama vile Mila na utamaduni, wanawake kutojiamini, utekekelezaji hafifu wa sera za kimataifa na kitaifa, ukosefu wa mazingira yanayovutia wanawake, ushirikiano mdogo kutoka kwa makundi makuu kama wanawake wenyewe, sera ambazo hazizingatii masuala ya kijinsia na kadhalika. Hivyo basi leo katika Ukumbi wa Wanawake tutajaribu kuangalia kuchambua kwa kina hali halisi ya ushiriki wa wanawake katika siasa katika ngazi mbalimbali.