Shughuli ya kutangaza moyo wa Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC yafanyika Zanzibar, Tanzania
2022-10-28 09:12:55| CRI

Shughuli ya kutangaza moyo wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC ilifanyika tarehe 26 mwezi Oktoba huko Zanzibar, Tanzania. Shughuli hiyo yenye kauli mbiu “Safari mpya yenye mustakabali wa pamoja” iliandaliwa na Idara ya lugha za Asia na Afrika iliyo chini ya Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG) ikishirikiana na Ubalozi mdogo wa China huko Zanzibar pamoja na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.

Filamu za documentary za lugha ya Kiswahili zilizotengenezwa na CMG zilioneshwa kwenye shughuli hiyo, ikiwa ni pamoja na “Kutegua Siri za Miaka Kumi na Mabadiliko ya China” “China yaanza safari mpya, dunia inanufaika pamoja na fursa mpya”.

Maofisa mbalimbali wa serikali ya Zanzibar, vyombo vya habari 17 vikiwa ni pamoja na TBC, ZBC, “Daily News” “Uhuru” “Zanzibar Leo” na wageni zaidi ya 40 walishiriki kwenye shughuli hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya Zanzibar Bibi Fatma Hamad Rajab na Naibu Katibu Mkuu wake Bw. Khamis Said walipongeza mafanikio ya Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC. Fatma ameipongeza CPC kwa kuongoza China kupata mafanikio makubwa, na kusema uzoefu wa maendeleo wa China unastahili kuigwa na nchi za Afrika, matokeo ya Mkutano huo yataleta fursa mpya ya maendeleo kwa uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika hasa Tanzania.

Kwa upande wake, Bw. Said alisema mpango wa maendeleo ya China na “Dhana ya uchumi wa bluu ya 2020-2050” ya Zanzibar zina mambo yanayofanana, ambapo pande zote mbili zinafuatilia njia ya maendeleo yenye “kushikilia kujitegemea na kujiamulia mambo” “kuhimiza moyo wa kujiamini kiutamaduni” “kuzidisha kuwanufaisha wananchi”, na zinaweza kuhimiza zaidi ushirikiano wa kivitendo.

Wanahabari wa Tanzania walioshiriki kwenye shughuli hiyo wanaona kuwa uzoefu wa utawala wa China unaziletea nchi za Afrika mfano wa kuigwa, na kutarajia China na Afrika zitanufaika pamoja na fursa mpya ya maendeleo.

Balozi mdogo wa China huko Zanzibar Bw. Zhang Zhisheng alieleza matokeo makuu na maana kubwa ya Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC, pamoja na athari yake kubwa kwa maendeleo ya uhusiano kati ya China  na Afrika. Alisema katika zama mpya China inataka kuendelea kuimarisha na kuzidisha mshikamano na ushirikiano na Tanzania, na kujenga kwa pamoja jumuiya imara zaidi yenye mustakabali wa pamoja ya China na Afrika.

Vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na TBC, ZBC na “Zanzibar Leo” viliripoti shughuli hiyo.