Samia kuwa rais wa kwanza wa nchi ya Afrika kupokelewa na China baada ya Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC
2022-10-28 09:13:44| CRI

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania atakuwa rais wa kwanza wa nchi ya Afrika kupokelewa na China baada ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC.

Kwa mujibu wa mwaliko wa rais Xi Jinping wa China, Rais Samia atafanya ziara ya kiserikali nchini China kuanzia tarehe 2 hadi 4 Novemba.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning jana alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa inaaminika kuwa ziara hiyo ya rais Samia itaingiza nguvu mpya ya uhai kwa uhusiano wa nchi hizo na kuhimiza maendeleo mapya katika ushirikiano wa kirafiki wa pande mbili.

Alieleza kuwa Tanzania ni nchi muhimu katika Afrika Mashariki na China na Tanzania zina urafiki wa jadi, na zimezidisha hali ya kuaminiana kisiasa, kushirikiana kivitendo na kuzaa matunda, na kudumisha ushirikiano mzuri katika masuala ya kimataifa na kikanda katika miaka ya hivi karibuni.

Mao aliongeza kuwa kanuni ya Udhati, Matokeo Halisi, Upendo na Nia njema iliyotolewa na Rais Xi katika ziara yake nchini Tanzania mwaka 2013 sasa imekuwa kanuni ya msingi inayoongoza ushirikiano kati ya China na nchi nyingine zinazoendelea.

Katika ziara ya Rais Samia, Rais Xi Jinping atafanya sherehe ya kumkaribisha na tafrija, na marais hao wawili watafanya mazungumzo na kuhudhuria kwa pamoja sherehe ya kutia saini nyaraka za ushirikiano.