Mawaziri wa mambo ya nje wa China na Marekani wazungumza kwa njia ya simu
2022-10-31 16:30:48| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi na mwenzake wa Marekani Bw. Antony Blinken leo wamezungumza kwa njia ya simu na kubadilishana mawazo juu ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili kwa sasa na siku za baadaye.

Bw. Wang Yi amesema Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China ni mkutano wa mshikamano, demokrasia na maendeleo. Taarifa muhimu zilizotolewa na Mkutano huo kwa nje ni kuwa China itaendelea kufuata kanuni za sera ya kidiplomasia za kulinda amani ya dunia na kuhimiza maendeleo ya pamoja, kuendelea kufuata sera ya msingi ya kufungua mlango, kutafuta maendeleo ya pamoja ya binadamu kwa njia ya China ya mambo ya kisasa, na kutoa fursa mpya kwa dunia kwa maendeleo mapya ya China. Wang amesema kama Marekani ikipenda kuielewa China, inapaswa kusoma kwa makini ripoti ya Mkutano huo. China inaitaka Marekani iache kutumia mtazamo mbaya na upendeleo wa kiitikadi kuiangalia China.

Kwa upande wake, Bw. Blinken amesema Marekani inafuatilia kwa karibu Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC na ripoti ya mkutano huo. Marekani inapenda kudumisha mawasiliano juu ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika siku za badaye, kufanya ushirikiano na kujadili msingi wa uhusiano wa nchi hizo mbili.

Aidha, juu ya suala la Ukraine, Bw. Wang Yi amezitaka pande zote husika zijizuie na kufanya juhudi za kidiplomasia ili kuepusha hali izidi kuwa mbaya.