AU yalaani shambulizi la kigaidi nchini Somalia
2022-10-31 08:43:51| CRI

Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililotokea katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, jumamosi, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 100 na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Mwenyekiti huyo pia amesema Umoja wa Afrika unatoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu, na kusema Umoja huo unasimama pamoja na serikali na watu wa Somalia katika wakati huu mgumu.

Jumapili, rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema, milipuko miwili ya mabomu yaliyotegwa kwenye magari iliyolenga jengo la Wizara ya Elimu nchini humo ilisababisha vifo vya watu 100 na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa. Amesema huenda idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na majengo ya ofisi kadhaa za serikali, hoteli na migahawa kuwa karibu na eneo la tukio.