Wataalamu wa China na Tanzania: Ziara ya Rais Samia nchini China kuinua uhusiano wa nchi hizi mbili kwenye ngazi mpya
2022-11-01 10:11:02| CRI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini China kuanzia kesho tarehe 2 hadi tarehe 4 mwezi Novemba, akiwa ni mkuu wa kwanza wa nchi ya Afrika kuizuru China baada ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC). Kwenye semina ya kimataifa kuhusu ziara ya rais Samia nchini China na mustakbali wa uhusiano kati ya China na Tanzania iliyoandaliwa Oktoba 31 na Taasisi ya Utafiti wa Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, wataalamu na wasomi wa China na Tanzania wote wanaona kuwa ziara ya Rais Samia itainua uhusiano wa nchi hizo mbili kwenye ngazi mpya. 

Akitaja matarajio yake kwa ushirikiano kati ya China na Tanzania, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang Prof. Liu Hongwu amesema pande hizo mbili zinapaswa kutilia maanani umuhimu wa kimkakati, kimsingi na kiuongozi wa ushirikiano kati ya China na Tanzania, na kuitumia vyema fursa inayotokana na ziara ya Rais Samia wa Tanzania nchini China ili kuinua uhusiano wa nchi hizo mbili hadi kufikia ngazi mpya, haswa kuimarisha hali ya kuaminiana kisiasa na mawasiliano kati ya vyama vya siasa vya nchi hizo mbili. Amesema China na Tanzania zote zimedumisha maendeleo tulivu kwa muda mrefu, hali inayoweka msingi imara kwa pande hizo mbili kubadilishana uzoefu kuhusu utawala wa nchi. 

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Humphrey Moshi amepongeza mafanikio ya Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC. Amesema ziara ya Rais Samia nchini China ni alama ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Tanzania na China, na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili una mustakbali mkubwa kwenye miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwemo maboresho ya Reli ya TAZARA na muunganiko kati ya bara la Afrika na kisiwa cha Zanzibar. Anaamini kuwa uhusiano na urafiki kati ya Tanzania na China hakika utapanda hadi kwenye ngazi mpya kutokana na juhudi za pamoja za pande hizo mbili. 

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof. Aldin Mutembei, ambaye pia ni mkurugenzi mgeni wa Taasisi ya Confucius ya UDSM, amesema mawasiliano ya kielimu yanatoa mchango muhimu katika kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na China. Lugha ya Kiswahili imeanza kutumika kwenye mashirika ya kitaaluma ya China, hali iliyotandika njia kwa ushirikiano wa uchumi na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili. Amesema kwa upande wa Tanzania Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimesukuma mbele ushirikiano kati ya pande hizo mbili kwenye nyanja mbalimbali kupitia taasisi ya Confucius. Pia ameeleza matumaini yake kuwa ziara hiyo ya Rais Samia nchini China itatoa fursa nyingi kwa maendeleo ya uhusiano kati ya Tanzania na China, na kupanua zaidi ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.