Wanasayansi barani Afrika watoa wito wa suluhisho la asili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
2022-11-01 08:52:34| CRI

Wanasayansi barani Afrika wamesema kutumia vizuri rasilimali ya asili ya bara hilo, ikiwemo misitu ya kitropiki, mikoko ya pwani na ardhi ya mboji ni njia rahisi na endelevu ya kuwa na Afrika ya kijani na imara katika siku zijazo.

Wakizungumza katika kongamano lililowakutanisha wanasayansi, watunga sera, na wadau wa mazingira kutoka ngazi ya chini lililofanyika jijini Nairobi, Kenya, wanasayansi hao wamesisitiza kuwa kudhibiti mgogoro wa hali ya hewa unaotokea barani Afrika kunawezekana endapo mtaji wa asili uliopo utatumika pamoja na hatua za lazima za kuendeleza mifumo isiyo na uchafuzi mwingi wa hewa.

Kongamano hilo linalofanyika kabla ya Mkutano wa 27 wa Pande Zilizosaini Mkataba wa Baioanuwai (COP27) wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika nchini Misri kuanzia tarehe 6 – 18 mwezi huu, linajadili nafasi ya misitu na mifumo mingine ya kiikolojia katika kuharakisha mageuzi ya kijani barani Afrika.