Rais wa China akutana na waziri mkuu wa Pakistan
2022-11-02 16:29:55| cri

Rais Xi Jinping wa China leo asubuhi hapa Beijing amekutana na waziri mkuu wa Pakistan Bw. Shehbaz Sharif ambaye yuko ziarani nchini China.

Rais Xi amemkaribisha Bw. Sharif na kumshukuru kwa kutoa barua ya pongezi kuhusu kufanyika kwa mkutano mkuu wa 20 Chama cha Kikomunisiti cha China CPC. Amesema,China na Pakistan ni marafiki, wenzi na ndugu wakubwa. Katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizo mbili zinaungana mikono na kusonga mbele kwa pamoja wakati hali ya dunia ina mabadiliko mengi, ikionesha uhusiano mzuri kati yao.

Amesema China siku zote inachukulia uhusiano huo kutoka upande wa kimkakati, huku ikiiweka Pakistan katika kipaumbele cha diplomasia ya nchi zilizoko karibu. China inapenda kushirikiana na Pakistan kuinua kiwango cha ushirikiano wa pande zote na kimkakati, kuharakisha kuunda jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Pakistan katika zama mpya, na kutia nguvu mpya katika uhusiano wa ushirikiano wa kimkakati na kiwenzi wa hali zote kati ya nchi hizo mbili.

Bw. Sharif amesema anafurahia kuwa mmoja wa viongozi walioalikwa kutembelea China baada ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa 20 wa CPC wenye maana kubwa, ikionesha urafiki mkubwa kati ya Pakistan na China. Amempongeza Rais Xi kwa kuchaguliwa tena kuwa katibu mkuu wa kamati kuu ya Chama cha CPC. Amesema katika miaka kumi iliyopita, China imepata maendeleo yanayosifiwa kama maajabu ya zama hii chini ya uongozi bora wa rais Xi, huku ikishikilia sera za pande nyingi katika mambo ya kimataifa, kuhimiza mshikamano na ushirikiano na kutoa mchango muhimu kwa amani na maendeleo ya dunia na kuonesha mfano wa nchi kubwa inayowajibika.