Rais Xi Jinping wa China afanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania
2022-11-03 20:32:17| CRI

Rais Xi Jinping wa China leo amekutana na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye yuko ziarani nchini China katika Jumba Kuu la Mikutano ya Umma la Beijing.

Baada ya kuhudhuria sherehe ya kumkaribisha rais Hassan, marais hao wawili wamefanya mazungumzo wakikubaliana kuinua uhusiano wa nchi zao kuwa uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote.

Rais Xi Jinping amebainisha kuwa, rais Hassan ni mkuu wa kwanza wa nchi ya Afrika kupokelewa na China baada ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), hali inayodhihirisha wazi ukaribu wa uhusiano kati ya China na Tanzania na hadhi muhimu ya uhusiano kati ya China na Afrika kwenye diplomasia ya China. Amesema, kwenye ziara yake nchini Tanzania mwaka 2013, alitaja dhana ya udhati, matokeo halisi, urafiki na uaminifu inayotakiwa kushikiliwa wakati wa kufanya ushirikiano na nchi za Afrika, ambayo sasa imekuwa falsafa ya sera za msingi inayoelekeza ushirikiano kati ya China na nchi zinazoendelea. Amesema, katika hali mpya, kuendeleza uhusiano kati ya China na Tanzania si kama tu kunaendana na maslahi ya pamoja na ya muda mrefu ya nchi hizo mbili, na bali pia kuna umuhimu mkubwa katika kusukuma mbele ujenzi wa jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja katika zama mpya.

Rais Xi amemfahamisha Rais Hassan kuhusu mambo husika ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC). Ameainisha kuwa, kuanzia sasa jukumu kuu la CPC ni kuwashikamanisha na kuwaongoza watu wa makabila mbalimbali wa China kukamilisha ujenzi wa nchi ya kisasa ya kijamaa na kuelekea lengo la pili la miaka 100, na kusukuma mbele kwa pande zote ustawishwaji wa taifa la China kupitia njia ya ujenzi wa nchi ya kisasa yenye umaalumu wa China. Rais Xi amesema, kujenga nchi ya kisasa hakumaanishi kuwa ya kimagharibi. China imepata njia ya maendeleo inayoendana na hali halisi ya nchi. Ujenzi wa nchi ya kisasa wenye umaalumu wa China unajikita katika udongo wa China, unaendana na uhalisi wa China, na una umaalumu wa China. Amesema, Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Chama cha Mapinduzi (CCM) cha Tanzania vyote vinabeba jukumu la kihistoria la kustawisha Chama na nchi, na CPC kinapenda kuendelea kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na CCM, na kuunga mkono ufundishaji na uendeshaji wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere.

Rais Xi amesisitiza kuwa, China siku zote inauzingatia kimkakati uhusiano kati yake na Tanzania, na siku zote ni rafiki anayetegemeka kwa Tanzania. Pande mbili zinapaswa kufuata mwongozo wa Uhusiano wa Wenzi wa Kimkakati wa Pande Zote, kuratibu na kuendeleza ushirikiano wa kirafiki kwenye nyanja mbalimbali katika kipindi kijacho. Amesema, China inaiunga mkono kithabiti Tanzania kulinda mamlaka yake, usalama wake na maslahi yake ya maendeleo, kuiunga mkono kithabiti Tanzania kutafuta njia ya kujiendeleza inayoendana na hali halisi ya nchi, na inapenda kuendelea kuungana mikono kithabiti na Tanzania kwenye masuala yanayohusisha maslahi makuu na ufuatiliaji mkubwa wa upande mwingine. Rais Xi amesema, China inapenda kuendelea kupanua uagizaji wa bidhaa maalumu za Tanzania, kuyaunga mkono makampuni ya China kuwekeza na kuanzisha biashara nchini Tanzania, na kutoa misaada kadri inavyoweza kwa ajili ya maendeleo ya uchumi na jamii nchini Tanzania. China inapenda kubadilishana uzoefu na mbinu za kustawisha vijiji na Tanzania, na kuunga mkono maendeleo kwenye maisha ya watu wa Tanzania.

Rais Xi ameainisha kuwa, reli ya TAZARA ni mnara mkubwa wa urafiki kati ya China na Tanzania na kati ya China na Afrika. Wakati China yenyewe ilipokuwa bado ni nchi maskini, Wachina walijibana matumizi ili kuweza kuwasaidia ndugu wa Afrika kujenga reli ya TAZARA. Sasa China imeinuka kimaendeleo, tunatakiwa kufuata barabara falsafa ya udhati, matokeo halisi, urafiki na uaminifu wakati wa kuwasaidia marafiki wa Afrika kutimiza maendeleo kwa pamoja, na kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja katika zama mpya. Amesema, kuendeleza uhusiano kati ya China na Afrika kunapaswa kufuata bila kuyumba mwelekeo mkuu wa kuaminiana, kunufaishana, kufundishana na kusaidiana. China na Afrika zinapaswa kuendeleza desturi nzuri, na kuenzi “moyo wa ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Afrika”, na kuendelea kuzidisha na kusukuma mbele moyo wa kujituma wa kihistoria kwenye shughuli za urafiki wa China na Afrika. China inapenda kutoa fursa mpya zinazotokana na maendeleo yake kwa Afrika, kuharakisha utekelezaji wa Miradi Tisa, kuimarisha nguzo tatu za biashara, uwekezaji na fedha ikiongozwa na miradi ya miundombinu, na kukuza msukumo mpya wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili. Rais Xi amesema, China inapenda kushirikiana na Afrika katika kushikilia kanuni za msingi za mahusiano ya kimataifa, zikiwemo kanuni tano za kuishi pamoja kwa amani, kutekeleza kihalisi Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, kuongeza uwakilishi na sauti ya nchi zinazoendelea kwenye usimamizi wa dunia, na kutoa mchango mkubwa zaidi katika ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.

Rais Hassan amesema angependa kutoa pongezi za dhati kwa mafanikio ya Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC na kwa Rais Xi kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, kwa niaba ya CCM na serikali ya Tanzania. Amesema, Tanzania inaichukulia China kuwa rafiki wa kweli na muhimu zaidi na inapenda kutumia fursa hii ya kuanzisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote, kuimarisha ushirikiano halisi kwenye sekta mbalimbali na kuinua uhusiano wa nchi hizo mbili hadi kufikia kiwango cha juu zaidi na kuufanya uwe mfano wa kuigwa wa uhusiano kati ya Afrika na China katika zama mpya. Amesema, Tanzania itaendelea kuiunga mkono kithabiti China katika masuala nyeti yanayohusisha maslahi yake ya msingi, yakiwemo masuala ya Taiwan, Xinjiang, Hongkong n.k. Ametoa shukrani kwa China kusaidia maendeleo ya Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere akisema vyama sita vya kusini mwa Afrika vinatarajia kubadilishana uzoefu wa utawala wa nchi na China. Pia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono na kushiriki kwenye Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). Rais Hassan amesema Pendekezo la Maendeleo ya Dunia lililotolewa na Rais Xi limekuja wakati mwafaka ambalo linafaa kutatua changamoto zilizopo duniani. Tanzania inapenda kushirikiana na China katika kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.

Katika mazungumzo yao, marais hao wawili wamekubaliana katika masuala hayo:

Kuimarisha mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili na kuzidisha mabadilishano katika ngazi zote kati ya serikali za mitaa, taasisi za kutunga sheria na vyama vya siasa;

Kuinua kiwango cha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya pande hizo mbili, kuimarisha ujenzi wa pamoja wenye ubora wa juu wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja", kuhimiza ushirikiano wa uwezo wa uzalishaji, na kupanua ushirikiano wa kunufaishana katika sekta za usindikaji na utengenezaji, maendeleo ya kijani, uchumi wa kidijitali n.k;

Kuzidisha mawasiliano ya kati ya watu wa nchi hizo mbili, kuandaa “Mwaka wa Utalii na Utamaduni wa China na Tanzania” katika wakati ufaao, na kuhimiza mabadilishano kati ya wasomi na vyombo vya habari vya nchi hizo mbili;

Kushirikiana kwa karibu katika masuala ya kimataifa, kama vile mabadiliko ya tabianchi na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, na kutetea haki na uadilifu wa kimataifa na maslahi ya pamoja ya pande zote mbili.

Baada ya mazungumzo, marais hao wawili wameshuhudia kusainiwa kwa nyaraka za ushirikiano zinazohusu biashara, uwekezaji, ushirikiano wa maendeleo, uchumi wa kidijitali, maendeleo ya kijani, uchumi wa buluu n.k. Pia wametoa taarifa ya pamoja juu ya kujenga uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Tanzania.

Baada ya hayo, Rais Xi ameandaa tafrija ya kumkaribisha Rais Hassan katika Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing.