Sayansi tunaweza kusema kuwa imeleta mapinduzi makubwa duniani, ambapo imemsukuma binadamu mbele kwa kufanya uvumbuzi katika sekta mbalimbali iwe za afya, kilimo, biashara, viwanda na nyinginezo. Iwe ni simu janja katika mifuko yetu, dawa zinazowasaidia binadamu kuishi na kustawi au roketi ambazo zinapeleka binadamu angani, sayansi inafanya yote hayo yaweze kutokea. Hivyo ili kuenzi maendeleo haya, dunia imekuwa ikiadhimisha Siku ya Sayansi Duniani kwa Amani na Maendeleo kila mwaka katika, ifikapo Novemba 10.
Siku hiyo ilitangazwa rasmi na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa mwaka 2001. Siku ya kwanza ya Sayansi kwa Amani na Maendeleo iliadhimishwa Novemba 10, 2002, na mwaka huu inaadhimishwa miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. UNESCO imesema katika taarifa yake, kwamba Siku hii ya Sayansi Duniani kwa Amani na Maendeleo inaangazia jukumu muhimu la sayansi katika jamii na hitaji la kushirikisha umma kwa mapana katika mijadala juu ya maswala yanayobuka ya kisayansi. Pia inasisitiza umuhimu wa sayansi katika maisha yetu ya kila siku.
Kwa kuunganisha sayansi kwa ukaribu zaidi na jamii, Siku ya Sayansi Duniani kwa Amani na Maendeleo inalenga kuhakikisha kwamba wananchi wanafahamishwa kuhusu maendeleo ya sayansi. Pia inasisitiza jukumu la wanasayansi katika kupanua uelewa wetu wa sayari yetu ya dunia iliyo nzuri, dhaifu na tunayoiita nyumbani kwetu, na kufanya jamii zetu kuwa endelevu zaidi. Hivyo leo hii kama kawaida kwenye kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia “Ushiriki wa wanawake kwenye maendeleo ya sayansi duniani".