Maofisa wa Afrika wasema kupata ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni ajenda muhimu katika mkutano wa COP27
2022-11-04 08:28:38| CRI

Maofisa wa Afrika wamesema, kutolewa kwa fedha zitakazosaidia nchi za Afrika kukabiliana na mgogoro wa tabianchi itakuwa ni ajenda muhimu katika mkutano ujao wa 27 wa Nchi Zilizosaini Makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika nchini Misri kuanzia Novemba 6 hadi 18.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwaka 2022 ya Hali na Mwelekeo wa Mabadiliko barani Afrika, maofisa hao wamesema kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa hali ya hewa, bara la Afrika litakuwa katika nafasi nzuri ya kutafuta uungaji mkono wa kifedha na kiteknolojia unaohitajika kuongeza kasi ya mabadiliko ya kijani.

Ripoti ya Hali na Mwelekeo wa Mabadiliko barani Afrika imeeleza kuwa licha ya mchango wake mdogo katika utoaji wa hewa chafu duniani, Afrika inaathirika zaidi na majanga ya hali ya hewa, na hivyo kuwa tishio kwa mfumo wa ikolojia na maisha ya viumbe.

Akizungumza katika mkutano huo, rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Akinwumi Adesina amesema, mkutano wa COP27 unatoa fursa ya kuziba pengo la ufadhili lililovuruga nia ya Afrika ya kuwa na mabadiliko ya kijani.