Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia jana alasiri idadi ya vifo kutokana na ajali ya ndege iliyoanguka katika Ziwa Victoria imefikia 19. Waziri mkuu huyo aliyewasili kwenye eneo la ajali huko Bukoba amesema bado kuna abiria waliokuwa wamekwama kwenye ndege hiyo.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) mapema jana ilitangaza kuwa ndege hiyo ya Shirika la Precision Air aina ya ATR-48 yenye namba za usajili 5H-PWF ilipata ajali wakati wa kutua saa tatu kasorobo asubuhi ikitokea Dar-es-salaam kuelekea Bukoba ikiwa na jumla ya watu 43, wakiwemo abiria 39 na wafanyakazi 4.
Kazi ya uokoaji bado inaendelea na timu ya uchunguzi ikihusisha mafundi wa Precision Air na wataalamu wa TCAA imetumwa kushiriki kwenye kazi hiyo.