Mkutano wa tabia nchi wa Umoja wa mataifa (COP 27) wafunguliwa nchini Misri
2022-11-07 08:58:15| CRI

Mkutano wa 27 wa Umoja wa mataifa kuhusu tabia nchi (COP 27) umefunguliwa jana mjini Sharm El Sheikh Misri, na kwa mara ya kwanza ajenda ya fedha za fidia ya madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi itajadiliwa kwenye mkutano.

Kwenye ufunguzi wa mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Misri Bw. Sameh Shoukry ambaye ni mwenyekiti wa mkutano huo, amesema pande shiriki zimekubali kuwepo kwa ajenda ya fedha za fidia kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema kwenye mjadala fedha hizo zitahusu gharama zinazotokana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kama zile zinazohusu kuongezeka kwa kiwango cha bahari na joto kali.

Amesema nchi za Afrika ni wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi, na zimeonesha utayari wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, lakini zinahitaji uungaji mkono.