Mkutano wa 14 wa Nchi zilizosaini Mkataba wa Ramsar kuhusu Ardhi Oevu wapitisha Azimio la Wuhan
2022-11-07 08:48:55| CRI

Kikao cha ngazi ya juu cha mawaziri cha Mkutano wa 14 wa Nchi zilizosaini Mkataba wa Ramsar kuhusu Ardhi Oevu kimefungwa mjini Wuhan, China. Kikao hicho kimepitisha rasmi Azimio la Wuhan, likitoa wito kwa pande zote kuchukua hatua ili kuzuia na kugeuza hatari za kimfumo zinazotokana na kuvia kwa ardhi oevu kote duniani.

Azimio la Wuhan, likiwa ni matokeo makuu ya mkutano huo, linaainisha kuwa katika miaka 51 iliyopita tangu Mkataba wa Ramsar uliposainiwa, maeneo 2,466 muhimu ya ardhi oevu ya kimataifa yamewekwa, miji 43 ya ardhi oevu imetambuliwa, mipango 19 ya kikanda imeanzishwa na juhudi nyingi za kila upande zimefanywa kwa ajili ya kuhifadhi ardhi oevu, hata hivyo, eneo la ardhi oevu kote duniani limeendelea kupungua kwa asilimia 35.

Katibu mkuu wa Mkataba wa Ramsar Dkt. Musonda Mumba amesema, kupitishwa kwa Azimio la Wuhan kumeonesha kuwa pande zilizosaini mkataba huo zinatilia maanani uhifadhi wa ardhi oevu na zimechukua hatua zenye uvumbuzi, na anatarajia kuwa zitaendelea kushikana mikono na kufanya juhudi za pamoja, ili kuanzisha ushirikiano wa kimataifa wenye kiwango cha juu zaidi katika kuhifadhi ardhi oevu.