Rais wa Tanzania aagiza kuajiriwa kwa mvuvi aliyeokoa abiria wa ndege iliyoanguka Ziwa Victoria
2022-11-08 08:44:46| CRI

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kumwajiri mvuvi aliyeongoza kazi ya kuwaokoa abiria baada ya ndege waliyosafiria kuanguka katika Ziwa Victoria Jumapili asubuhi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu inasema, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kumwajiri mvuvi huyo anayejulikana kwa jina la Majaliwa Jackson kwenye Jeshi la Zima Moto na Uokoaji.

Vyombo vya habari vya huko vimesema mvuvi huyo aliwaongoza wenzake kuwaokoa abiria muda mfupi baada ya ndege hiyo kuanguka kando ya Ziwa Victoria, na jumla ya watu 24, wakiwemo abiria 22 na wafanyakazi wawili wa ndege waliokolewa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, abiria 17 na marubani wawili walifariki dunia baada ya ndege ya Shirika la Precision Air la Tanzania aina ya ATR-48 kuanguka ziwani Jumapili wakati ilipojaribu kutua kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba ikitokea Dar es Salaam.