China kuchukua hatua za kuboresha kazi ya kuzuia na kudhibiti janga la COVID-19
2022-11-10 20:43:47| CRI

Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) umefanyika tarehe 10 Novemba, ambapo umesikiliza ripoti ya kuzuia na kudhibiti janga la COVID-19, kujadili na kutangaza hatua 20 za kuboresha kazi ya kuzuia na kudhibiti janga hilo. Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya CPC Xi Jinping aliendesha mkutano huo na kutoa hotuba muhimu.

Kwa mujibu wa mkutano huo, hivi sasa virusi vinaendelea kubadilika, huku maambukizi ya virusi yakiendelea kuenea duniani. China ikiwa nchi yenye idadi kubwa ya watu, ina idadi kubwa ya watu walio katika makundi hatarishi, maendeleo ya sehemu mbalimbali hayana uwiano, na rasilimali za jumla za matibabu bado hazitoshi. Kutokana na mabadiliko ya virusi na hali ya hewa ya majira ya baridi, kuna uwezekano kuwa janga hilo litaweza kuenea zaidi, hivyo ni muhimu kudumisha hatua za kimkakati kuzuia na kudhibiti janga hilo kwa kisayansi na kwa usahihi.