Rais wa Ufaransa atangaza kukomeshwa kwa operesheni za kijeshi za Ufaransa katika eneo la Sahel
2022-11-10 08:57:51| CRI

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametangaza kuwa Ufaransa inakomesha operesheni ya kijeshi ya Barkhane kwenye eneo la Sahel la Afrika.

Akiongea mjini Toulon kusini mwa Ufaransa, Rais Macron amesema Ufaransa haitaendelea kuwepo kwenye eneo hilo bila ukomo, lakini ameongeza kuwa msaada wa kijeshi kutoka kwa Ufaransa kwa nchi za Afrika kwenye eneo la Sahel utaendelea kuwepo kwa njia nyingine.

Ufaransa ilituma karibu wanajeshi 5,100 katika nchi tano za Sahel (Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger) kwa lengo la kusaidia kulinda maeneo yao, na kuzuia eneo hilo kuwa ngome ya makundi ya kiislamu yenye msimamo mkali.

Ufaransa itajadiliana na wadau wake wa Afrika kuhusu mtindo wa msaada ya kijeshi, na hali ya sasa ya operesheni za vituo vya kijeshi vya Ufaransa katika eneo la Sahel na Afrika Magharibi.