Msumbiji kuanza kuuza nje gesi asilia iliyoyeyushwa kupitia mradi wa FLNG kaskazini
2022-11-14 09:42:55| CRI

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi Jumapili alitangaza kuwa Msumbiji imeanza kusafirisha nje gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG), wakati meli ya mafuta ya British Sponsor tayari imeondoka kwenye eneo la maji ya Msumbiji, ikiwa na shehena ya kwanza ya gesi hiyo inayozalishwa na mradi wa kaskazini mwa nchi hiyo Coral South Floating Liquefied Natural Gas (FLNG).

Ukiwa mradi mkubwa zaidi barani Afrika na wa pili duniani, Coral South FLNG ni sehemu ya utangulizi wa mradi wa gesi wa Kitalu cha 4 nchini Msumbiji, ambao ni ubia unaojumuisha kampuni za ENI ya Italia, ExxonMobil ya Marekani, CNPC ya China, ENH ya Msumbiji, Galp ya Ureno na KOGAS ya nchini Korea Kusini.

Katika mahojiano hivi karibuni na Shirika la habari la China Xinhua, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kitaifa ya Petroli ya Msumbiji Nazario Bangalane alisema mradi wa Coral South FLNG una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wa nchi hiyo, na usafirishaji wa shehena ya kwanza nje ya nchi ni mwanzo wa Msumbiji kuibuka kama mzalishaji na muuzaji nje wa gesi asilia iliyoyeyushwa katika soko la kimataifa.