Xi na Biden wafanya mazungumzo ya wazi na kina juu ya uhusiano wa nchi mbili na masuala makubwa ya kimataifa
2022-11-15 10:12:49| CRI

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Marekani, Joe Biden, walikuwa na mazungumzo ya wazi na ya kina jana Jumatatu kuhusu masuala yenye umuhimu wa kimkakati kwenye uhusiano kati ya China na Marekani na masuala makubwa ya kimataifa na kikanda.

Kwenye mazungumzo yao, Xi alisema hali ya sasa ya uhusiano wa China na Marekani haipo kwenye maslahi ya kimsingi ya nchi hizo mbili na watu wake, na haipo kama inavyotarajiwa na jumuiya ya kimataifa. China na Marekani zinahitaji kuwajibika kwa ajili ya historia, dunia na watu, kuchunguza njia sahihi ya kuishi pamoja katika enzi mpya, kuweka uhusiano kwenye njia sahihi, na kuurejesha kwenye njia nzuri na ukuaji utulivu kwa manufaa ya nchi hizo mbili na dunia kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa uhusiano wa China na Marekani haupaswi kuwa mchezo wa “nishinde usishinde”.Alisema China haitaki kubadili utaratibu wa kimataifa uliopo au kuingilia masuala ya ndani ya Marekani, na haina nia ya kupinga au kuiondoa Marekani, bali pande zote mbili zinapaswa kuheshimiana na kuishi pamoja kwa amani.

Xi pia alisema suala la Taiwan ni kiini cha maslahi ya China, msingi wa kisiasa wa uhusiano wa China na Marekani, na mstari wa kwanza mwekundu ambao haupaswi kuvukwa kwenye uhusiano wa China na Marekani. Na kwamba utatuzi wa suala la Taiwan ni mambo ya ndani ya China, na yeyote anayetaka kuitenganisha Taiwan na China atakuwa anakiuka maslahi ya kimsingi ya taifa la China.

Kwa upande wake Biden amempongeza Rais Xi kwa kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na kusema zikiwa nchi mbili kubwa, Marekani na China zina wajibu wa kuwa na uhusiano wa kiujenzi.

Amesema Marekani inadhamiria kufungua njia za mawasiliano kati ya marais hao wawili na katika ngazi zote za serikali, ili kuruhusu mazungumzo ya wazi juu ya masuala ambayo pande hizo mbili hazikubaliani, na kuimarisha ushirikiano unaohitajika na kubeba jukumu muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na changamoto nyingine muhimu duniani, ambazo ni muhimu kwa nchi hizo mbili na watu wake, na pia kwa dunia nzima.

Biden alisisitiza tena kuwa China yenye utulivu na ustawi ni nzuri kwa Marekani na dunia, akisema kuwa Marekani inaheshimu mfumo wa China, na haitaki kuubadilisha.

Amesema Marekani haitafuti vita vipya vya Baridi wala washirika dhidi ya China, haiungi mkono "Taiwan kujitenga," haiungi mkono "China mbili" au "China moja, Taiwan moja," na haina nia ya kuwa na mzozo na China. Serikali ya Marekani inafuata sera ya China moja, na haitaki kutumia suala la Taiwan kama chombo cha kuidhibiti China, ikitarajia kuona amani na utulivu katika Mlango Bahari wa Taiwan.