Bibi Peng Liyuan ahudhuria hafla ya wake wa viongozi wa Kundi la Nchi 20
2022-11-15 22:14:39| CRI

Bibi Peng Liyuan, mke wa rais Xi Jinping wa China Jumanne asubuhi alihudhuria hafla ya wake wa viongozi ya mkutano wa kilele wa Kundi la Nchi 20 (G20) kisiwani Bali, Indonesia, shughuli ambayo iliandaliwa na mke wa rais wa Indonesia Bibi Iriana Joko Widodo.

Wakati Bibi Peng alipowasili kwenye hafla hiyo, mke wa rais wa Indonesia Bibi Iriana alimkaribisha kwa ukarimu na kupiga naye picha pamoja. Bibi Peng na wake wengine wa viongozi wa G20 walitazama maonyesho ya ngoma za jadi za Bali na wakapiga picha pamoja.

Bibi Peng akiambatana na Bibi Iriana walitembelea maonyesho ya ala za muziki za kienyeji, mavazi, ufumaji wa vikapu, utarizi na chakula kisicho na kemikali, na pia alijaribu kutengeneza vitu vya sanaa za jadi za Kiindonesia, kama vile ufumaji wa majani ya mitende akipiga muhuri wa nembo ya Mkutano wa G20 na picha ya maua kwenye mfuko uliofumwa.

Bibi Peng alipongeza wazo la Indonesia la kuunganisha utengenezaji wa kazi za mikono na uwezeshaji wa wanawake, na kupunguza umaskini na kuhifadhi mazingira. Alisema China na Indonesia zinaweza kuimarisha ushirikiano na mawasiliano katika sekta husika na kutoa mchango katika juhudi za kikanda za kupunguza umaskini na kuhifadhi mazingira.