Tanzania yaanza kuchunguza kikamilifu ajali ya ndege Ziwa Victoria
2022-11-15 10:15:22| CRI

Msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amesema serikali imeanza uchunguzi kamili kuhusu chanzo cha ajali ya ndege iliyotokea katika Ziwa Victoria Novemba 6 na kusababisha vifo vya watu 19, na kuongeza kuwa Baraza la Mawaziri lililokutana mjini Dodoma liliagiza wataalamu wa masuala ya anga kuungana na wenzao wa kimataifa katika uchunguzi huo.

Msigwa aliwaambia wanahabari baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ripoti ya kwanza ya uchunguzi huo itatolewa ndani ya siku 14 ikifuatiwa na ripoti ya awali itakayotolewa ndani ya siku 30 na ripoti ya mwisho kutolewa ndani ya miezi 12.

Alisema Baraza la Mawaziri pia limeagiza mamlaka zote za usimamizi wa maafa ziimarishwe ili kuziwezesha kukabiliana na maafa zikiwemo ajali.

Msigwa alisema Baraza la Mawaziri lilitoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwani uchunguzi unaendelea na taarifa kamili ya uchunguzi huo itawekwa wazi.