China yafuatilia suala la usalama wa chakula duniani
2022-11-16 10:16:47| CRI

China inapenda kuendelea kushirikiana na nchi mbalimbali duniani katika kuimarisha usalama wa chakula na kupunguza umaskini.

Hayo yalisemwa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bibi Mao Ning jana kwenye mkutano na waandishi wa habari alipojibu maswali kuhusu Kongamano la kimataifa la “Utoaji wa msaada wa mpunga chotara kwa nje na usalama wa chakula duniani” lililofanyika Novemba 12 mjini Beijing, China.

Mao alisema utafiti wa mpunga chotara unatoa mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa chakula na maendeleo ya kilimo kwa nchi nyingi duniani, na kuchangia ufumbuzi wa China katika kutatua suala la uhaba wa chakula kwa nchi zinazoendelea.

Aliongeza kuwa China inafuatilia sana suala la usalama wa chakula duniani. Rais Xi Jinping wa China ametoa Pendekezo la Maendeleo Duniani na kuufanya usalama wa chakula kuwa sehemu ya sekta kuu nane za ushirikiano. China inapenda kuendelea kushirikiana na nchi mbalimbali duniani katika kuhimiza Pendekezo la Maendeleo Duniani, kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya usalama wa chakula na kupunguza umaskini, na kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuharakisha kutekeleza Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 na kujenga dunia isiyo na njaa na umaskini.